Dodoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetoa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 68 wa kada ya Uhandisi na Fundi Sanifu ikiwa ni hatua muhimu ya kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na ufanisi katika kuhudumia wananchi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika ukumbi wa Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma yakilenga kuwajengea uelewa watumishi hao kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na maadili yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Azimina Mbilinyi amesema kuwa mafunzo hayo ni msingi muhimu wa kuwajengea uwezo watumishi wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uwazi na uzingatiaji wa maadili ya kazi.
Bi. Azimina amewataka watumishi hao kufuatilia kwa makini mada zinazotolewa ili kupata maarifa yatakayowawezesha kuwa watumishi bora na wenye mchango chanya katika maendeleo ya sekta ya barabara za vijijini na mijini.
Katika mafunzo hayo washiriki wamepatiwa mada mbalimbali zinazohusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Aidha, walikula viapo vya uadilifu wa utumishi wa umma vilivyoongozwa na Mhadhiri wa Chuo cha Utumishi wa Umma Bw. Martine Fute.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha watumishi hao kuanza majukumu yao wakiwa na uelewa mpana jambo litakalosaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na TARURA.